1 Corinthians 14

1Utafuteni upendo na kutamani sana karama za rohoni, zaidi sana mpate kutoa unabii. 2Maana yeye anenaye kwa lugha hasemi na watu bali husema na Mungu. Maana hakuna aelewaye kwa sababu anena mambo yaliyofichika katika Roho. 3Lakini yeye atoaye unabii, asema na watu na kuwajenga, kuwatia moyo, na kuwafariji. 4Yeye anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, lakini yeye atoaye unabii hulijenga kanisa.

5Sasa natamani kwamba ninyi nyote mnene kwa lugha. Lakini zaidi ya hayo, natamani ya kwamba mtoe unabii. Yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha (labda awepo wa kutafasiri), ili kwamba kanisa lipate kujengwa. 6Lakini sasa, kaka na dada zangu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini ninyi? Siwezi, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya maarifa, au unabii, au kwa njia ya fundisho.

7Ikiwa vitu visivyo na uhai kama filimbi au kinubi visipotoa sauti zilizo na tofauti, itatambulikanaje ni chombo gani kinachezwa? 8Kwa maana ikiwa baragumu itatoa sauti isiyojulikana, ni jinsi gani mtu atatambua ya kuwa ni muda wa kujiandaa kwa vita? 9Vivyo hivyo na ninyi. Mkitoa kwa ulimi neno lisilo dhahiri, ni jinsi gani mtu ataelewa mnachosema? Mtakuwa mkiongea, na hakuna atakayewaelewa.

10Hakuna shaka kwamba kuna lugha nyingi mbalimbali duniani, na hakuna hata moja isiyo na maana. 11Lakini ikiwa sijui maana ya lugha, nitakuwa mgeni kwake yeye anenaye, naye anenaye atakuwa mgeni kwangu.

12Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani sana kuona uthihirisho wa Roho, takeni kwamba mzidi sana kulijenga kanisa. 13Hivyo, yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kutafasiri. 14Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.

15Nifanye nini? Nitaomba kwa roho yangu, lakini pia nitaomba kwa akili zangu. Nitaimba kwa roho yangu, na nitaimba kwa akili zangu pia. 16Vinginevyo, ukimsifu Mungu kwa roho, yeye aliye mgeni ataitikaje “Amina” utoapo shukurani, akiwa hayajui usemayo?

17Maana ni kweli wewe washukuru vema, lakini yule mwingine hajengwi. 18Namshukuru Mungu kwa kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote. 19Lakini katika kanisa ni heri ninene maneno matano kwa ufahamu wangu ili nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.

20Kaka na dada zangu, msiwe watoto katika kufikiri kwenu. Badala yake, kuhusiana na uovu, iweni kama watoto wachanga. Lakini katika kufikiri kwenu mkawe watu wazima. 21Imeandikwa katika sheria, “Kwa watu wa lugha nyingine na kwa midomo ya wageni nitasema na watu hawa. Wala hata hivyo hawatanisikia,” asema Bwana.

22Hivyo, ndimi ni ishara, sio kwa walioamini, bali kwa wasioamini. Lakini kutoa unabii ni ishara, sio kwa wasioamini, bali kwa ajili yao waaminio. 23Haya, ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja na wote wanene kwa lugha, na wageni na wasioamini wameingia, je hawawezi kusema kwamba mna wazimu?

24Lakini ikiwa wote mnatoa unabii na asiyeamini au mgeni akaingia, atashawishiwa na yote asikiayo. Atahukumiwa na yote yasemwayo. 25Siri za moyo wake zingefunuliwa. Matokeo yake, angeanguka kifudifudi na kumwabudu Mungu. Angekiri ya kwamba Mungu yu kati yenu.

26Nini kifuatacho basi, kaka na dada zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana Zaburi, mafundisho, mafunuo, lugha au tafsiri. Fanyeni kila kitu ili kwamba mlijenge kanisa. 27Kama yeyote ananena kwa lugha, wawepo wawili au watatu, na kila mmoja katika zamu. Na mtu lazima atafasiri kilichosemwa. 28Lakini kama hakuna mtu wa kutafasiri, basi kila mmoja wao akae kimya ndani ya kanisa. Basi kila mmoja aongee peke yake na kwa Mungu.

29Na manabii wawili au watatu wanene, na wengine wasikilize kwa kupambanua kilichosemwa. 30Lakini aliyeketi akifunuliwa jambo katika huduma, yule ambaye alikuwa ananena na anyamaze.

31Kwa kuwa kila mmoja wenu anaweza kutoa unabii mmoja baada ya mwingine ili kwamba kila mmoja aweze kujifunza na wote waweze kutiwa moyo. 32Kwa kuwa roho za manabii ziko chini ya uangalizi wa manabii. 33Kwa kuwa Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani. Kama ilivyo katika makanisa yote ya waumini,

34imewapasa wanawake wakae kimya katika kanisa. Kwa kuwa hawaruhusiwi kuzungumza. Badala yake, wanapaswa kuwa katika unyenyekevu, kama pia sheria inavyosema. 35Kama kuna chochote wanatamani kujifunza, basi wawaulize waume zao nyumbani. Kwa kuwa ni aibu kwa mwanamke kuongea katika kanisa. 36Je neno la Mungu lilitoka kwenu? Je limewafikia ninyi tu?

37Kama mtu akijiona kuwa ni nabii au wa rohoni, inampasa ayatambue mambo ninayowaandikia ya kwamba ni maagizo ya Bwana. 38Lakini asipotambua haya, mwacheni asitambuliwe.

39Hivyo basi, kaka na dada zangu, takeni sana kutoa unabii, na msimzuie mtu yeyote kunena kwa lugha. Lakini mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.

40

Copyright information for SwaULB